Wednesday, January 23, 2019


N’NOLEWAPO

Mengi yamekuja, kwa kweli na yamepita,
Mazuri yakaja, na mabaya yakapita,
Wa kuninoa kaja, kazi kutekeleza,
Kuninoa menoa, kwa kweli men’noa.

Majuto kawa mengi, mbona uhai upo?
Kili yangu kaijaza, kufa kungalipo,
Wa bua wangu moyo, kashindwa kustahimili,
Kuninoa menoa, kwa kweli men’noa.

Mapito ya duniya, na uzito katukia,
Kaja kama gharika, kwa mpango kunangusha,
Mtima ‘ghadhabisha, ghanima kanangushia,
Kuninoa menoa, kwa kweli men’noa.

Kapata wa kunifaa, ya dunia kurahisisha,
Nkagaza mfunulia, siri ya wangu mtima,
Nkakingisa kwa kung’ang’ana, ila nifike wapi,
Kuninoa menoa, kwa kweli men’noa.

Wakati ulipowadia, kashindwa kustahimili,
Kajaribu kufa kingoto, lakini ngo! Sikuweza,
Yote kanilemea, kaona heri kuyafichua,
Kuninoa menoa, kwa kweli men’noa.

Kakaa kitako kwa kinoo, n’nolewe n’noleke,
Kamfichulia yote ya moyo, bila hata bakshishi,
Sikio kanipa bambam, kabaini yalonipausha,
Kuninoa menoa, kwa kweli men’noa.

Nami nisemeni, kwa kwako kujitolea,
Mekuwa mhibu, kanondolea mikwala,
Mjio wako kwangu, kawa ni faraja kweli,
Kuninoa menoa, kwa kweli men’noa.



No comments:

Post a Comment