Makala


MAKALA YALIYOWASILISHWA KWENYE KONGAMANO LA SITA KATIKA CHUO KIKUU CHA CHUKA
UKWELI-KINZANI KATIKA UWASILISHAJI WA MOTIFU YA SIRI KATIKA KAZI ZA NATHARI ZA FASIHI YA KISWAHILI: MIFANO KUTOKA KWA NATAKA IWE SIRI NA SITAKI IWE SIRI
BEATRICE NYAMBURA NJERU
CHUO KIKUU CHA CHUKA
0700625372
PROF. JOHN KOBIA
CHUO KIKUU CHA CHUKA
0720809725
Ikisiri
Motifu ni dhana muhimu katika kuelewa fasihi. Motifu ni kipengele cha kijadi kinachohusu kurudiwarudiwa kwa wazo au dhamira fulani katika sehemu kubwa ya kazi za fasihi hususan riwaya, tamthilia, ushairi na fasihi simulizi. Makala haya yanalenga kuchunguza motifu ya siri katika kazi teule za nathari za fasihi ya Kiswahili. Dhana ya siri ni kikale ambacho kimekuwepo katika jamii mbalimbali kuanzia zamani. Kikale hiki kingali kinajitokeza katika kazi za fasihi kama ilivyo katika kazi zilizoteuliwa.  Dhana hii inaweza kurudiwa katika kipengele cha matumizi ya lugha, mbinu za uandishi, dhamira ya mwandishi, usawiri wa wahusika na uendelezaji wa masuala makuu. Mojawapo ya mbinu zinazotumiwa kuwasilisha motifu ya siri ni ukweli-kinzani. Hivyo, makala haya yatachunguza namna mbinu ya ukweli-kinzani imetumika kuwasilisha dhana ya siri katika Nataka Iwe Siri na Sitaki Iwe Siri. Sampuli maksudi itatumika kuteua vitabu viwili kwa msingi kuwa vina dhana ya siri katika uteuzi wa mada. Pia, vitabu hivi, ambavyo ni Nataka Iwe Siri na Sitaki Iwe Siri vimedhihirisha mbinu ya ukweli-kinzani moja kwa moja katika uteuzi wa mada zake. Uchanganuzi na uwasilishaji wa data itakayopatikana kutokana na usomaji wa kazi teule utakuwa wa kimaelezo. Makala haya yatawafaa wahakiki kwa kuwapa mwanga wa namna ya kuhakiki kazi zinazohusiana na siri. Aidha, walimu na wanafunzi wa viwango vyote watafaidika kwa kuwa wataelewa kazi zilizoteuliwa zaidi. Waandishi nao, watanufaika kutokana na makala haya kwa kuwa watayatumia kama nyenzo kutunga kazi za baadaye za kiwango cha juu zaidi kuhusiana na motifu ya siri. Vilevile makala haya yatatoa mchango mkubwa katika taaluma ya fasihi ya Kiswahili kwa kuwa yataongezea maarifa mapya kuhusu namna mbinu ya ukweli-kinzani inavyotumika kukuza wahusika na kujenga motifu mbalimbali zinazojitokeza katika nathari za fasihi ya Kiswahili.
Maneno makuu: Ukweli-kinzani, motifu, motifu ya siri na nathari ya kiswahili


1. Utangulizi
Kazi hii inaangazia matumizi ya mbinu ya ukweli kinzani katika ujenzi wa motifu ya siri katika kazi teule za nathari za fasihi ya Kiswahili ambazo ni Nataka Iwe Siri na Sitaki Iwe Siri.  Ukweli kinzani ni mtindo ambao mwandishi hubuni muktadha ambao una ukweli na vilevile ukweli huo una ukinzani (Kilonzo na Masaku 2017). Hivyo, mbinu ya ukweli kinzani huwa na maneno yanayopingana katika kazi ya fasihi. Maneno haya yanayopingana huwa yanatolewa kwa pamoja ili kusisitiza ujumbe fulani. Mada za kazi zilizoteuliwa kwa uchunguzi ili kufanikisha uandishi wa ripoti hii zimetumia mbinu ya ukweli kinzani. Kirumbi (1971) anaendeleza motifu ya siri kwa kuwatumia wahusika mbalimbali ili kuficha siri na wengine kufichua siri zao. Kwa upande mwingine, Matundura (2008) anatumia wahusika wake kujenga motifu ya siri ila sasa baadhi ya wahusika wale wanataka iwe siri na wengine hawataki iwe siri. Hali hii ya baadhi ya wahusika kutaka siri iwe siri na wengine kutaka kufichua siri imetumia mbinu ya ukweli kinzani, jambo ambalo linaendelezwa katika sehemu ya uchanganuzi wa data katika makala haya. Dhana ya siri katika kazi teule imeendelezwa hadi kufikia kiwango cha kuwa motifu.
Motifu ni kipengele cha kijadi kinachohusu kurudiwarudiwa kwa wazo au dhamira fulani katika sehemu kubwa ya kazi za fasihi hususan riwaya, tamthilia, ushairi na fasihi simulizi (Mulokozi 1996). Kurudiwarudiwa kwa dhamira fulani katika kazi ya fasihi humfanya msomaji kuyapata barabara maudhui ambayo mtunzi wa kazi hiyo ametaka wasomaji wake wayapate. Mulokozi ametaja aina kadhaa za motifu zikiwemo; motifu ya safari, motifu ya msako, motifu ya mama wa kambo, motifu ya bikizee na motifu ya mtoto kigego wa maajabu anayezaliwa na kuanza kuongea. Motifu ya siri ni matumizi ya mbinu ya kuficha mambo yanayojitokeza na kujirudiarudia katika kazi ya fasihi na hivyo kuitawala kazi hiyo ya fasihi (Karama na wengine 2018). Katika jamii, yapo mambo yanayoendelezwa kisirisiri. Baadhi ya mambo haya ni kama vile matumizi ya siri katika dini, siasa, mbinu za kujitajirisha na pia matumizi ya siri katika njia za kuhifadhi na kuendeleza utamaduni wa kijamii (Yenjela 2015).
Wamitila (2002), anaeleza kuwa vikale vinaweza kuwa taswira, wahusika, miundo ya usimuliaji na kadhia nyingine zinazopatikana katika fasihi popote pale ulimwenguni. Vikale humwezesha mhakiki wa fasihi kubainisha uhusiano uliopo kati ya fasihi za aina mbalimbali. Waitifaki wa nadharia ya vikale wanashikilia kwamba umaarufu wa kazi ya sanaa unatokana na maudhui na taswira zinazorudiwa katika kazi ile. Asili ya aina hii ya uhakiki ni saikolojia na visasili. Kadhalika, Wamitila (keshatajwa) anasema kuwa fasihi zina sifa ambazo huzipa uwezo wa kiulinganishi hivi kwamba msingi wa fasihi duniani ni jamii zilizoundwa na binadamu. Kwa hivyo, fasihi mbalimbali duniani huingiliana na mwingiliano katika masuala yanayohusu maisha ya binadamu ndio huwezesha fasihi kulinganishika. Pia, ulinganisho huu hutokana na sababu kwamba fasihi zote ulimwenguni hutumia lugha kama malighafi yao na lugha zote duniani huwa na sifa zinazofanana. Aidha, fasihi zote duniani huchota maudhui yake kutoka katika jamii za wanadamu.


2. Mwauo wa maandishi
Motifu ya siri katika kazi za fasihi ya kiswahili
Karama, Mutiso na Chimerah (2018), wanaeleza kuwa utenzi wa Siri La Asrari ulitungwa kwa kuendeleza motifu ya siri. Kutokana na uhakiki wa Karama na wenzake utenzi huu ulitungwa na Mwanalemba na unazungumzia vita alivyopigana Mtume Muhammad aliyekuwa nabii wa waislamu dhidi ya Andharuni ambaye anasawiriwa kuwa adui wa waislamu. Awali, Mtume Muhammad alishindwa na Andharuni kwa kuwa iliaminika kuwa, ushindi wa Andharuni ulitokana na siri ya hirizi iliyokuwa kichwani mwake iliyompa nguvu za kiajabu. Hatimaye, Mtume anafanikiwa kuipata hirizi hiyo kupitia kwa msaada wa ndege na kumshinda adui yake. Uhakiki wa Karama na wengine (keshatajwa) unaeleza kuhusu motifu ya siri jambo ambalo litaangaziwa katika makala haya. Uhakiki huu utasaidia kufafanua na kuielewa zaidi motifu ya siri. Hata hivyo, uhakiki huu ni tofauti na uhakiki wa sasa kwa kuwa umeangazia motifu ya siri katika utanzu wa ushairi lakini utafiti huu utaangazia matumizi ya mbinu ya ukweli kinzani katika kuendeleza motifu ya siri katika kazi za nathari za fasihi ya Kiswahili ukiwemo utanzu wa riwaya na fasihi ya watoto.
Matundura (2018), ameeleza kuhusu motifu ya siri. Ametoa maelezo kuhusu vitabu mbalimbali vya fasihi ya Kiswahili vinavyoendeleza motifu ya siri katika kukuza dhamira na maudhui ya waandishi wa kazi hizo. Kazi alizozitaja Matundura ni; Ushairi wa Siri La Asrari, Sitaki Iwe Siri, Nataka Iwe Siri, Siri ya Ging’ing’i na Siri Sirini 1, 2 na 3. Alipendekeza kuwa, motifu ya siri iangaziwe katika kazi zile kwa kuangalia kama kazi hizo zinaingiliana ama kutofautiana kimtindo na kimaudhui ili kutoa mchango katika fasihi ya Kiswahili. Makala haya yalihusu motifu ya siri katika fasihi ya Kiswahili, suala ambalo litaangaziwa katika uhakiki huu. Aidha, makala haya yatafaa uhakiki huu kwa kuwa yatatoa mwelekeo wa uteuzi wa sampuli ya kutafitiwa. Kando na maelezo ya Matundura, uhakiki huu utapiga hatua zaidi na kuangazia matumizi ya mbinu ya ukweli kinzani katika ujenzi wa motifu ya siri katika kazi za nathari za fasihi ya Kiswahili.
Vikale katika kazi za fasihi ya kiswahili
Njogu na Wafula (2007: 81-82), wakiwanukuu Jung (1972) na Cuddon (1997) wanadai kuwa Jung, akifanya utafiti juu ya njozi na ndoto, alichukulia kikale kama aina ya mtiririko au picha kongwe inayojitokeza mara kwa mara katika tajriba anayopitia mwanadamu. Wanashikilia kwamba, mtu na utamaduni wake ni nakala ya wanadamu wengine waliokuwepo kabla yake miaka mingi iliyopita na hivyo kuwa kikale. Maoni ya Jung ni kwamba hata kama utu wa mtu ni wa kibinafsi, mtu huathiriwa na jamii inayomzunguka. Hawezi kamwe kuepukana na athari zake. Maelezo haya yatasaidia uhakiki huu kwa kuwa yatasaidia katika uelewa wa matumizi ya vikale katika kazi za fasihi.
Gathara (2015) naye akimnukuu Werner (1968) katika uchunguzi wa visasili na visakale vya wabantu alithibitisha uhusiano uliopo katika mila, desturi na lugha zao, dhana ya kuwepo kwa Mungu mmoja, licha ya kwamba wengine hawatofautishi baina ya mawingu na jua, kuamini katika maisha ya baada ya kifo na kuwa na mawazo kwamba roho za waliokufa zinaweza kuathiri hali zao za kimaisha kwa kiwango chochote kile. Kutokana na maelezo haya, ni wazi kuwa katika kulinganisha visasili, visakale na matambiko ya jamii tofautitofauti, kuna uhusiano katika ruwaza za visasili na matambiko katika tamaduni za jamii mbalimbali na kwamba tamaduni hizi za binadamu huwa vikale. Maelezo ya Gathara kuhusu uhusiano kati ya visasili, visakale na matambiko utasaidia uhakiki huu kwa kuwa utaeleza uhusiano uliopo baina ya kikale cha tamaduni za jamii mbalimbali ulimwenguni. Kwa hivyo, utafiti wa Gathara utafaa uhakiki huu kwa kuwa utaweza kueleza kwa mapana tofauti zinazojitokeza katika uendelezaji wa masuala tofautitofauti kutegemea mazingira ya waandishi mbalimbali kupitia kwa mbinu ya ukweli kinzani.
3. Msingi wa kinadharia
Uhakiki huu utaongozwa na Nadharia ya Vikale. Vikale ni picha kongwe zinazotokea mara kwa mara katika kazi za fasihi (Abrams 1981). Abrams anazidi kufafanua kuwa chimbuko la nadharia hii hutoa maelezo yake kuwili. Kwa upande mmoja, chimbuko la nadharia hii ni kwenye kazi ya George Frazer ya The Golden Bough (1890-1915). Kazi hii huchunguza ruwaza ya sifa za visasili na matambiko ambayo anadai kuwa hufuatilia ruwaza ya kimsingi inayojirudiarudia katika visakale na taratibu nyingine katika tamaduni mbalimbali za binadamu kote ulimwenguni. Kwa upande mwingine, Abrams (mtaje) aneleza kuwa nadharia ya vikale ilitokana na maelezo ya Gustav Jung kuhusu akili-laza. Jung alitumia istilahi ya vikale kwenye taswira za asili za kumbukumbu zinazorudiwarudiwa kutokana na tajriba katika maisha ya zamani ili kutilia mkazo akili-laza jumuishi. Alieleza kuwa, taswira hizi hurithishwa kutoka kwa kizazi kimoja hadi kingine na kutiwa kwenye akili-laza jumuishi ya jamii ya watu na ambazo hujitokeza katika visasili, mawazo ya binadamu, dini na ndoto katika vipengele vyote vya maisha ya binadamu na pia katika kazi za fasihi.
Eagleton (1983) anaeleza kwamba, kazi za fasihi huwa kwa kiwango fulani zimeandikwa tena na waandishi ambao mara nyingi huwa hawatambui kwamba wameandika kazi zao kama kazi za wengine. Kwa kusema haya, anamaanisha kuwa, hakuna usomaji wa kazi ambayo ni ya asili; kila usomaji huwa wa kusoma kazi ambayo imeandikwa tena. Haya yanatokana na hali ya uambukizanaji. Kwa hivyo, vikale vinaweza kuonekana kwa viwango mbalimbali, viwe ni vya kimaudhui, kitaswira, kimatumizi ya lugha au vya ujenzi wa wahusika na kufanana kutoka kwa kazi moja au nyingine. Nadharia ya uhakiki wa vikale inaeleza kuwa binadamu wote ni sawa popote walipo (Mutiso 1999). Tofauti ni ndogo na za kufikiria ambazo husababishwa na tofauti ndogo za kihistoria na za kimazingira. Vikale kwa jumla hurejelea ruwaza za kimsingi ambazo aghalabu hudhihirika katika jamii za watu mbalimbali duniani. Miongoni mwa wataalamu ambao wamezungumzia nadharia hii ni Northrop Fyre (1957) na Carl Jung (1957) kama anavyodai Coyle na wengine (1990: 51).
Nadharia ya vikale, kutokana na sifa bia zake zinazotokana na vikale katika fasihi, itakuwa yenye manufaa katika uhakiki huu kwa kuwa itaongoza katika uchunguzi wa namna mbinu ya ukweli kinzani imetumika kuendeleza vikale mbalimbali kikiwemo kikale cha siri na utamaduni kama ilivyojitokeza katika kazi teule za nathari za fasihi ya Kiswahili na kukuza uwasilishwaji wa wahusika pamoja na uendelezaji wa masuala makuu.


4. Uchanganuzi na uwasilishaji wa data
Ukweli kinzani katika Nataka Iwe Siri
Mukhtasari wa Nataka Iwe Siri
Nataka Iwe Siri ni riwaya ya Kiswahili iliyoandikwa na Kirumbi mwaka wa 1971. Riwaya hii inaangazia kipindi cha wakati wa mkoloni na hata baada ya mkoloni kuondoka nchini Tanzania na kuonyesha masuala makuu mbalimbali katika jamii yakiwemo masuala ya siri katika ulezi, mapenzi, ndoa, uchawi, elimu, maendeleo, kazi, umoja na ushirikiano, urafiki, ulevi, kifo na uadilifu. Masuala haya yameendelezwa kwa kina na wahusika kama vile Mzee Hadiswele, Mzee Tingisha, Mwamtoro, Namcheja, Chiku, Msiba, Dizelu, Dikulu, Hanatama, Havijawa na Bi. Kigola. Wahusika hawa wamechorwa na mwandishi kwa taswira tofauti ili kufanikisha ujenzi wa dhamira ya mwandishi pamoja na masuala makuu. Dhamira ya mwandishi ni kuhusu umuhimu wa kuficha na kufichua siri. Vilevile, ameonyesha mchango wa wazazi katika uamuzi wa wanandoa kwa wana wao. Ameonyesha vile wahusika wanaweza kuathirika na kuficha na kufichua siri zao. Baadhi ya wahusika wameficha siri zao hadi kaburini huku wengine wakizifichua. Athari za kufichika kwa siri kama anavyoonyesha Kirumbi ni ukosefu wa raha na furaha na kifo. Nazo athari za kufichuka kwa siri kama anavyozidi kueleza ni kama vile kuzuka kwa ugomvi, kuzuka kwa chuki, kujua ukweli na kusameheana. Kando na haya, mwandishi ametumia mbinu tofauti za uandishi na za lugha na kuandika kazi inayovutia sana. Mbinu hizi zimetumiwa kimwafaka na kufanikisha uendelezaji wa siri hadi ikafikia kiwango cha kuwa motifu. Mojawapo wa mbinu zilizotumika kufanikisha utunzi wa kazi hii ni mbinu ya ukweli kinzani. Mbinu hii inajitokeza katika kazi hii na imejadiliwa kwa mapana.

Ukweli kinzani katika Nataka Iwe Siri
Siri ni kikale kinachojitokeza katika kazi za fasihi. Kikale hiki kilikuwepo tangu jadi ambapo marafiki wangeamua kufichiana siri au kufichuliana siri. Kuficha siri na kufichua siri katika jamii huwa ni hiari ya mtu. Kazi hii ya Kirumbi imeonyesha kuwa, kufichika au kufichuka kwa siri kunategemea anayefichiwa au kufichuliwa siri hiyo. Kwa hivyo, ikiwa mhusika anataka kuiweka siri yake, lazima awe na sababu zake za kuificha siri hiyo na ikiwa anataka kuitoboa, lazima awe na sababu zake za kutaka kuitoboa. Hata hivyo, ni lazima achunguze kwa kina yule anayemtobolea siri zake. Katika kazi hii, motifu ya siri imeendelezwa kama ifuatavyo na mbinu ya ukweli kinzani:
Wakati wa mkoloni, kijiji cha Chalambe kilikuwa nyuma kimaendeleo kikilinganishwa na kijiji cha Mbagala. Sababu za kuwa nyuma kwa kijiji hiki zilijulikana na mkoloni mwenyewe. Kwanza, mkoloni aliwaona watu wa kijiji cha Chalambe kuwa wabishi, wasiofaa kuendelezwa na waliofaa kuchukiwa sana. Matokeo ya chuki hii yaliwaletea maumivu makali huko jela na wakadaiwa kodi bila kuelimishwa sababu, faida na kazi ya kodi hiyo. Nia ya kufanya hivi ilikuwa siri kwa mkoloni ya kuwafanya watu wa Chalambe wadharauliwe na kukosana ili watawanyike. Siri ya kutawanyika huku ilikuwa ni kuweza kutawaliwa vizuri. Hata hivyo, ukweli kinzani unajitokeza kama ifuatavyo:
“… badala ya watu wa Mbagala kuwadharau watu wa Chalambe au watu wa Chalambe kuwaonea wivu watu wa Mbagala, vijiji hivi viwili kwa pamoja vilisaidiana kutengeneza barabara kubwa kwa njia ya msaragambo na kufanya mengi kwa kujitolea kwa lengo la kujitegemea.” (Ukurasa 1)
Vilevile, watu walilazimishwa kulima pamba na wakoloni na baada ya ulimaji huo, mkoloni alikusanya pamba hiyo kupitia kwa njia ya maakida na kuiuza. Badala ya kuwapa wanachalambe haki yao, kila mtu alipata bahashishi ya senti thelathini na tano kwa kazi ya mwaka mzima. Zaidi ya udhalimu huo, mkoloni alichukia mila na tamaduni za wanachalambe na kuvuruga mila hizo kupitia kwa maakida. Hiki kikawa ndicho kisasili cha kufukuzwa kwa maakida kutoka Chalambe. Inaaminika kuwa akida wa mwisho alichomewa nyumba yake na Chalambe ikaishi bila maakida hadi ilipopata uhuru.
Aidha, ukweli kinzani unadhihirika katika urafiki kati ya Chiku na Msiba. Vijana hawa wawili walikuwa kielelezo katika jamii. Wote walikuwa na maadili mema na walikuwa wameelimika. Ilisadifu kuwa kila mmoja alizaliwa kama mtoto wa pekee kwa wazazi wao. Chiku alikuwa binti ya Mzee Hadiswele na Mwamtoro naye Msiba alikuwa bin Dizelu na Namcheja. Wazazi wa kike wa watoto hawa waliitana muhile yaani wale watu wawili ambao watoto wao wanataka kuoana au wameoana. Kisadfa, wana wale wawili walianzisha uhusiano ambao ulijulikana na mama zao. Kina mama waliufurahia uhusiano ule. Baada ya wawili wale kuhusiana kwa muda walipanga kuoana. Inaonekana kuwa maamuzi yao yalikuwa mazuri na ya heri kwa wazazi wao. Hata hivyo, ukweli kinzani unadhihirika mwandishi anaposema kuwa;
“Urafiki ulipozidi kukua, waliamua kuoana. Maamuzi hayo kati yao wenyewe hayakutosha, kinyume chake yangaliwaletea shida na magumu.” (Ukurasa 14)
Swali ni, kwa nini maamuzi yale yangewaletea shida na magumu ilhali kina mama wa watoto hawa tayari walikwisha ukubali uhusiano wa watoto hao. Hiyo ilibakia kuwa siri hado ilipoanza kufichuka.
Hatimaye, Msiba alimteua Dikulu aliyekuwa rafiki yake kwa muda ili awe mshenga katika posa kati ya Chiku na Msiba. Alipomfikia Mzee Hadiswele, alimwambia kuwa wao wameamua kuja kwake ili kuomba undugu. Kisha alimkabidhi Hadiswele barua ya posa. Hadiswele anapoipata ile barua, kinyume kinatendeka. Badala ya kufurahia kuwa bintiye amekwisha mpata mwanamume mwenye maadili, elimu na kazi ya kutajika anakasirika.
“Mzee Hadiswele alipokea hiyo barua, akaipindua pindua akawa anacheka na kuguna. Mzee alionyesha kama amechanganyikiwa… Sijui niseme nini! Sikutazamia haya nikikwambia kweli, wala mpaka sasa siamini masikio yangu wala siamini macho yangu.” (Ukurasa 5)
Baadaye, Mzee Hadiswele na Dikulu wanaagana na Dikulu anaondoka kwa Mzee Hadiswele. Mzee Hadiswele alipoifungua barua na kuanza kuisoma;
“… moyo ulimwuma na akajuta kwa nini aliifungua na kuisoma. Machozi yakawa yanamlengalenga, na mawazo yake hayakutulia… Msiba amwoe Chiku, haitawezekana.” (Ukurasa 5)
Mwandishi anaonyesha kuwa katika jamii hii kulikuwa na mila kuhusu uamuzi wa wazazi kwa mambo yanayohusu ndoa za wanao. Kwamba, ili pasiwe na shida na ugumu wowote katika ndoa za wana ni lazima wazazi wote wangekubaliana na uchumba huo. Hata hivyo, katika Nataka Iwe Siri kuna ukinzani wa uamuzi wa wazazi wa Chiku. Huku mama yake akiufurahia uchumba wa Chiku na Msiba na kutaka waoane, Mzee Hadiswele ameshtuliwa na uchumba huo na kusema kuwa wale wawili hawawezi kuoana kwa sababu ambazo yeye mwenyewe anataka ziwe siri. Anapomweleza mkewe kuhusu ombi lile la posa, mama Chiku anaonekana kana kwamba ameifurahia sana posa hiyo. Naye Mzee Hadiswele badala ya kufurahia anaanza kuzungumza kuhusu Mzee Kauchape kulea wajukuu anaowaona kuwa haramu. Je, yeye pia anamlea mtoto haramu na hajui? Hiyo ni siri. Kisha, Mama Chiku anamwuliza sababu za kutotaka Chiku na Msiba waoane na jibu analolitoa ni;
“Hataolewa naye! Iwapo mimi ndiye baba yake, hataolewa naye… Lolote nalitokee lakini mimi sitakubali Msiba amwoe Chiku. Sitaki leo hadi kesho, hata niwapo kaburini. Na iwapo utakuwepo mpango wowote kinyume changu, basi Chiku sina radhi naye.” (Ukurasa 8)
Maneno haya yanamchoma moyo Mama Chiku anayeyaona kuwa siri ya mtungi aijuaye kata. Aidha, mwandishi anaeleza kuwa kuna siri ya moyoni ambayo aijuaye tu ni mwanasiri mwenyewe ambaye ni moyo. Kwa hivyo, Mama Chiku anaiona siri ya Mzee Hdiswele kuwa siri sirini kwa kuwa ni siri inayoifadhiwa moyoni ambao pia ni siri kwa vile hakuna mtu hata mmoja wakiwemo madaktari anayeweza kuijua siri iliyo moyoni au jambo lililo moyoni hata baada ya kuupasua. Mama Chiku hachoki kumdadisi mumewe kuhusu sababu za kutoa ule uamuzi. Udadisi unapozidi, Mzee Hadiswele anapandisha mori na kuona kuwa kumekuwa na wanaume wawili katika nyumba hiyo. Mama Chiku anafanikiwa kumtuliza ila hajaridhika na uamuzi wa mumewe wa kuwakatalia wanao uchumba. Mzee Hadiswele anapoona kuwa wawili hao watabishana kwa muda mrefu anasema;
“…Jambo moja nijualo ni kwamba moyo wangu mzito kwa sababu ya posa hii, nami sipendi Chiku aolewe na Msiba. Hiyo ndiyo siri ya moyo wangu, na nataka iwe siri.” (Ukurasa 9)
Chiku, kupitia kwa mamake, anagundua kuwa baba yake alikataa posa iliyoletwa na Dikulu kutoka kwa Msiba. Anaamua kumwuliza baba yake sababu za kumkataa mchumba wake Msiba. Jibu linalotoka kinywani mwa Mzee Hadiswele lina ukweli kinzani. Anasema;
“Msiba ni msiba, ukimkosa msiba, na ukiolewa naye ni msiba. Kati ya misiba hiyo ailetayo Msiba, nimeamua kufuata msiba uitwao msiba… ajionaye kuwa fundi wa kubishana mimi namruhusu kugombania ubunge ili apiganie haki za wanawake bungeni lakini sio ndani humu.” (Ukurasa 11)
Kwa hivyo, badala ya baba Chiku amweleze bintiye sababu nzuri za kuukataa uchumba kati yake na Msiba, anaanza kuwa mkali na kutumia mabafu kuwakataza wale wawili kuoana bila kujua kuwa hakuna aliye na uwezo wa kuzuilia mapenzi kati ya wawili wapendanao kama anavyosema Dikulu.
Hatimaye, kukataliwa kwa posa kati ya Chiku na Msiba kunamwangaisha Chiku. Analia usiku wote na kuujaza mto wake kwa machozi. Keshoye anapoenda kazini, walimu wenzake wanang’amua kuwa Chiku ana kasoro na hata anapewa ruhusa mapema ili aende nyumbani. Badala ya kwenda nyumbani, Chiku anaelekea kwa Msiba na kumkuta akitayarisha chamcha. Chiku anaomba msamaha kwa Msiba na kumwambia kuwa hataweza kumsaidia na kazi za pale nyumbani ila kula tu. Katika harakati hizo, Msiba anagundua kuwa Chiku ana neno na hivyo anamuuliza Chiku kilichojiri ila Chiku hataki kumwelezea. Msiba anapodadisi zaidi, Chiku anasema;
“Msiba, jana sikulala; na kukosa usingizi ndiko kulikonifanya niwe hoi kiasi cha kuruhusiwa kuondoka shuleni. Wewe uliniletea nyuki. Msiba, na hao nyuki waleta msiba mtupu sasa.” (Ukurasa 13)
Msiba anashangaa ni vipi posa yake ya heri njema imegeuka na kuwa nyuki wanaoleta msiba. Kwake, alidhania kuwa posa ile ingeleta furaha kati yake na Chiku kwa kuwa walikuwa wanapendana kwa dhati lakini posa ile imegeuka na kuwa nyuki wa kuleta hasara ya msiba badala ya kutoa asali. Hata ingawa Chiku anazungumza kwa mafumbo, Msiba anaweza kuyang’amua mafumbo hayo kutokana na uvumbuzi wake wa haraka. Wawili hawa wanaanza kutafuta suluhu baada ya kukataliwa kwa posa na Msiba anamshauri Chiku kuwa wasiingie katika uchafu lakini wamwachie Mungu yote.
Kwa upande mwingine, Mzee Hadiswele alienda kwa rafikiye Tingisha aliyekuwa mshenga wake ili amwombe ushauri na kumtuma aende azungumze na Mama Chiku kuhusu ndoa kati ya Msiba na Chiku na kumwambia Mama Chiku amuunge mkono ili waweze kuikataa ndoa ile. Hadiswele anapoenda kwa Tingisha inatarajiwa kuwa, kwa kuwa ni mzee mwenzake na rafiki yake wa dhati, atamfichulia siri ya sababu ya kukataa posa ya Msiba. Tingisha anamwomba amweleze sababu za kuikataa. Anasema;
“Sasa mimi nikusaidie nini Hadiswele? Maana hujanipa mwanya wowote wa kukushauri, maana angalau ungenieleza sababu zako, hapo ningekuwa na la kusema.” (Ukurasa 18)
Tingisha mwenyewe amechanganyikiwa na hajui ampe ushauri upi mwenzake. Kumbe hata marafiki wa dhati wanaweza kufichiana siri. Ili kuujibu usemi wa Tingisha, Hadiswele anasema;
“Ndugu moyo wangu mzito katika shauri hili lote, na siri ya uzito nataka iwe siri.” (Ukurasa 18)
Tingisha anamshauri asiwe na uzito wa kutoboa siri ili hatimaye asije akastukia kuwa ndoa ya siri kati ya vijana hao imepitishwa. Hadiswele anaanza kupandisha mori na kusema kuwa, Tingisha kumchokoachokoa Hadiswele hakuna maana bali anafaa aende amshawishi Mama Chiku ili abadili mawazo yake ili wao wazungumze kwa sauti moja.
Baada ya kutoka kwa Tingisha, Hadiswele alifululiza hadi kwa Namcheja, mamake Msiba, ili ashauriane naye pia. Anapofika kule, Namcheja anashtushwa na mjio wake kwani ulikuwa umepita muda mrefu kabla ya Hadiswele kumtembelea Namcheja. Lengo la safari hii ni kumwomba Namcheja amshawishi Msiba ili ndoa kati yake na Chiku isifanikiwe. Baada ya ubishi wa muda, Namcheja anamwambia Hadiswele kuwa, Chiku na Msiba wanakubaliwa kuoana kisimba kwa simba. Hadiswele anazidi kumweleza kuwa mila za aina ile zimepitwa na wakati na zinahitaji kuvunjwa na kutungiwa sheria mpya. Ndiposa Namcheja anamwuliza Hadiswele iwapo yeye, yaani Hadiswele, alitaka Namcheja amfichulie Msiba siri. Je, ni siri gani? Hadiswele anamjibu;
“La, hiyo siri na nataka iwe siri na ibaki kuwa siri… Hilo ndilo nisilolitaka. Nimekwambia nataka iwe siri hata hivyo sioni uhalali wa hao watoto wangu wote wawili waoane.” (Ukurasa 20)
Katika kauli hii ukweli kinzani unatokea kwa sababu kilichowafanya Chiku na Msiba wasioane ni kujua ukweli kuwa wote ni wa baba mmoja, yaani Mzee Hadiswele, kama anavyofikiria lakini Hadiswele bado anataka iwe siri. Hadiswele anafikiria kuwa Namcheja anataka kulipiza kisasi dhidi ya Hadiswele kutoenda kwa Namcheja mara kwa mara kumtembelea baada ya kufiwa na mumewe aliyekuwa baba wa bandia wa Msiba. Namcheja anaona kuwa Hadiswele alimkosesha kwa kumfanya auvunje uaminifu wake kindoa kwa mumewe marehemu Dizelu na kwa mke wa Hadiswele. Anakiri kuwa watoto wao wamezaliwa kwa hatia na kusema;
“Wasipooana lawama ni yetu na wakioana lawama ni yetu. Na katika haya makosa mawili lazima tupate kuchagua kosa moja tulifanye tukijua kuwa tunakosa, yaani tuendelee kuongeza kosa juu ya kosa.”
(Ukurasa 20)
Wawili hawa, badala ya watafute suluhu ya kukosoa kosa walilolitenda, wanaamua kuendelea kukosea ili kusuluhisha kosa bila kufahamu kuwa kosa haliwezi kusuluhishwa kwa kutenda kosa lingine. Hofu inaanza kumwingia Hadiswele. Anaona kuwa;
“… akiwazuia watoto hao kuoana wataoana kwa siri na akiwaruhusu pia atakuwa bado hajazuia haramu, unyumba wake si busara kwani jina lake linaweza kuchafuka.” (Ukurasa 21)
Mwandishi anaeleza kuwa siri ya nguvu ya siri ni kuwa, siri hupata nguvu zake wakati hofu inapoingia ya kutotaka mambo yajulikane. Aidha anasisitiza kuwa;
“… ushupavu wa siri ni upumbavu wa mwana siri afichaye siri yenye uhusiano na uovu. (Ukurasa 21)
Kutokana na maelezo haya, Hadiswele anapiga moyo konde na kusema kuwa;
“Maji yaliyomwagika hayazoleki, lakini waweza tu kukausha sakafu na kuchota mengine mtungini…” (Ukurasa 21)
Hadiswele anasema maneno haya akimwomba Namcheja azungumze na muhile wake, Mwamtoro, ili wote washirikiane kuikomesha ndoa kati ya Msiba na Chiku. Namcheja anakubaliana na Hadiswele ila siri iliyo moyoni mwake ya kukubali kule haijulikani.
Wakati Hadiswele alikwenda kwa Namcheja, naye Tingisha alienda kwa Mwamtoro. Maneno ya Mwamtoro yalimtingisha Tingisha badala ya Tingisha kuyatingisha. Mwamtoro alimtingisha Tingisha kwa maneno kwa kuwa alikiri kuwa Chiku si mtoto wa Hadiswele na haya Tingisha aliyafahamu vizuri kuwa yeye, yaani Tingisha, ndiye baba halali wa Chiku. Mwamtoro anaeleza zaidi kuwa Hadiswele alikuwa baba yaya wa Chiku kwani ajuaye mtoto ni wa nani ni siri ya mama mtoto. Kwa hivyo, kwake Mwamtoro, haoni sababu ya Chiku na Msiba kutooana kwa kuwa Chiku si mwanawe Hadiswele. Mwamtoro anamwuliza Tingisha iwapo anataka aitoboe siri naye Tingisha anasema;
“Kama nilitaka iwe siri, hadi sasa nataka iwe siri. Na kwa siri, nakwambia kuwa mtoto huyu asiolewe na msiba.” (Ukurasa 22)
Haya hayadhihirisha kuwa Tingisha ana hofu ya siri yao kujulikana lakini bado anazidi kuongezea siri ndani ya siri. Wawili hawa wanakinzani kimsimamo kuhusu siri yao. Tingisha anapotishiwa na Mwamtoro kuwa siri itatobolewa na isikae kati ya wana tu bali mambo yajulikane hadharani naye Tingisha akatae hayo hadharani, Tingisha anasema;
“Mambo haya tuliyafanya yawe sirini na nataka yaendelee kuwa siri.” (Ukurasa 22)
Mwamtoro anaendelea kushikilia kuwa;
“Hakuna siri wakati huu tena maadamu mnataka kuwaonea hawa vijana. Kijiji chote kitayafahamu mambo haya msipojihadhari… Iwapo unataka ibaki kuwa siri itakubidi umshawishi rafikiyo akubali posa ya Chiku. Lakini iwapo utamwacha akaze uzi, mimi nitaukata, sote tupate hasara.” (Ukurasa 22)
Hatimaye, wahile wale wawili walikutana pia na kufichuliana siri. Namcheja alimweleza Mwamtoro kuwa Msiba alikuwa mwana wa Hadiswele naye Mwamtoro akamwambia Namcheja kuwa Chiku alikuwa mwana wa Tingisha. Hapo ndipo Mwamtoro alipomtuma Namcheja aende akamwelezee Hadiswele kuwa watoto wale wawili si ndugu na kuwa ilimbidi Hadiswele awaruhusu kuoana. Ukweli kinzani unatokea pale ambapo marafiki wa dhati wanasalitiana hadi kufikia kiwango cha kuchangiana wanaume.
“Ama sisi tumekuwa mashoga, mpaka tunachangiana mabwana!” (Ukurasa 28)
Baadaye, Namcheja anaamua kumwambia ukweli Hadiswele kuwa Chiku hakuwa mtoto wake bali alikuwa mtoto wa rafikiye Tingisha. Anapofichuliwa siri hii, Hadiswele anasema;
“Siri njema iwapo inataka yenyewe iwe siri. Lakini hata ukitaka iwe siri, siri ikikataa kuwa siri matatizo yatakuandama katika kuifukia na hali yenyewe yajifukua. Uchafu haufutiki kwa kutojulikana na wengine. Udhalimu hauondoki kwa kutotajwa wala kweli haibadiliki kuwa uwongo ati kwa kuwa inauma. Ushupavu au udume katika ukweli hauonekani katika kufunika kweli, bali katika kuifunua hata iwe inamwambua msemaji… Asiyejua ukweli, mpe ukweli. Aliyetaka kweli mpe kweli maadamu anaihitaji.” (Ukurasa 29)
Mwishowe, Hadiswele anamwita Tingisha, Namcheja na Mwamtoro nyumbani kwake siku iliyofuata jioni baada ya siri kufichuka na anakubali Msiba na Chiku waoane kwa kuwa si siri tena. Hata hivyo, anawataka wanasiri wenzake waiweke siri hiyo na wanawekeana agano la milele kuwa hawatakubali kutokuwa waaminifu katika ndoa tena. Hadiswele anaamini kuwa, kwa hakika hakuna siri ya kweli. Hatimaye, Hadiswele anamwita Chiku, Msiba, Mwamtoro, Dikulu, Tingisha na Namcheja nyumbani kwake ili kuwapa ujumbe kuwa sasa amekubali posa ya Msiba na kuwa wale wawili wanaweza kuoana. Hapa, mbinu ya ukweli kinzani inajitokeza ili kuijenga motifu ya siri. Badala ya wachumba hawa kufurahia kwa kuwa wataoana na hatimaye wataanza kuishi pamoja, Chiku anasimama taratibu hadi chumbani kwake na kurudi na pete mkononi na pia kijifurushi. Alipoingia alimkabidhi Msiba ile pete na lile furushi na kusema;
“Si vyema kusema haya lakini yanibidi. Msiba alinivalisha pete ya uchumba kwa siri majuma mawili yamepita, leo namrudishia. Na kifurushi hicho ni jumla ya zawadi alizonipa wakati wa uchumba wetu. Leo nimerudisha kama alama dhahiri ya kuvunja uchumba wetu. Hapa namalizia. Nami narejea ndani. Sababu sina, lakini huo ndio ukweli wa moyo wangu.” (Ukurasa 37-38)
Maneno haya yalipafanya mahali pale pawe kama palipomwagiwa maji kwani kila mtu alipumbaa. Hayo hayakuwa matarajio yao.
Kando na hayo, Chiku alipoenda kwa Msiba siku baada ya babake kuikataa posa ya Msiba alimwambia kuwa penzi lake kwa Msiba si kibatali ambacho kingezimika upepo uvumapo katika ukurasa wa 14. Hata hivyo, kuna ukweli kinzani unaodhihirika kupitia kwa ushairi anaoutunga Msiba anaporudi kwake baada ya Chiku kuuvunja uchumba wao. Katika kibwagizo cha ushairi huo anasema;
“Penzi kama kibatali, ghafla kunizimikia.” (Ukurasa 38)
Analilinganisha penzi la Chiku na kibatali ambacho upepo unapovuma ghafla kinazimika. Anaona kuwa Chiku ameukataa uchumba wao kutokana na vile ambavyo Hadiswele alikuwa amekataa posa yake na anayaona maneno haya kama kinyume na alivyokuwa amwemwahidi Chiku kuwa;
“Mapenzi yangu si yale ya kibatali, upepo ujapo basi yazimike. Niaminivyo mimi, yatubidi tuoane.”
(Ukurasa 14)
Mama Chiku anamrai Chiku anamtobolee siri ya kuukataa uchumba wake na Msiba. Anamwambia kuwa anafaa kumtobolea mamake siri kwa kuwa ni msiri na hata anajua siri ya kuwepo kwake duniani. Kwa kujibu rai ya mama yake, Chiku anasema;
“Mama nimekwambia toka usiku wa jana kama ipo sababu, mimi siijui, au ni siri kiasi cha kuifanya itoke itabomoa badala ya kujenga.” (Ukurasa 41)
Naye mamake anazidi kumbembeleza kwa maneno yanayotumia mbinu ya ukinzani na kusema;
“Chiku, dunia hii mambo huwa sirini kwa kitambo tu, baada ya muda yale yaliyofichika hufichuliwa. Yaliyokuwa gizani na sirini, huja nuruni tena hadharani. Siri huondoa raha na furaha. Na ukiwa sirini jinsi hiyo utakosa furaha maishani, na maisha raha yake ni kuwa na furaha.” (Ukurasa 41)
Hata baada ya Mama Chiku kumwambia Chiku maneno haya, Chiku bado hajashawishika kumfichulia mamake siri iliyo sirini. Anampiga chenga kwa maneno yafuatayo;
“Kama maisha yamekusudiwa furaha, na kama mtu hapati furaha, nini faida ya kuishi? Furaha ya kweli katika dunia hii haipatikani. Na sitapata furaha ya aina yoyote kwa kuolewa na Msiba kama nilivyofikiria awali. Na sitambui kama yeye angelipata furaha kunioa. Na kwa kuwa nampenda Msiba, nimeamua kutoolewa naye. Kuolewa naye atajuta mwenyewe na kutotaka kuwaamini tena wanaadamu hasa hao marafiki wake na hao awapendao.” (ukurasa 41)
Badala ya Chiku kuitoboa siri ili apate raha na furaha, alitaka kuididimiza siri sirini katika siri. Mwishowe, Chiku alimwahidi mamake kuwa atawafichulia siri ya kukataa uchumba wa Msiba mtondogoo asubuhi. Matumaini ya kufichua siri ile yalimaliza ugomvi nyumbani kwa Mzee Hadiswele. Jioni hiyo, baada ya kazi, Chiku alienda kuonana na rafiki yake Hanatama. Wawili hao walizungumza mengi na hata Chiku alimfahamisha Hanatama kuwa aliuvunja uchumba kati yake na Msiba. Hakumfichulia siri ya kuvunjika kwa uchumba huo bali alimtuma Hanatama ampelekee Msiba barua aliyomwomba amfikishie kesho kutwa wala si keshoye. Hanatama aliishuku ile barua na kushangaa ni kwa nini barua ile ichelewe kufikishwa lakini Chiku bado aliifanya kuwa siri na kumwambia kuwa akiipeleka barua hiyo keshoye ataharibu kila kitu. Je, ni kitu gani? Atakiharibu kwa namna gani? Kutokana na urafiki wao, Hanatama alikubali ombi la Chiku.
Siku hiyo baada ya kazi, chiku alipitia kwa Bi. Kigola aliyeaminika kuwa mchawi mkali pale kijijini pao. Alimwomba Bi. Kigola ampe vidawa na akapewa. Baadhi ya vidawa alivinywa akiwa hapo kwa Bi. Kigola na vingine akavinywia nyumbani. Pana ukweli kinzani kuwa Bi. Kigola alimpa Chiku dawa iliyomuua na hata yeye mwenyewe hakufichuliwa siri ya sababu za kujiua kwa Chiku. Hatimaye, Chiku katika ile barua anamuaga Msiba na kumwachia msiba badala ya mapenzi na siri aliyotaka iwe siri ikawa siri hadi kaburini. Katika ushairi uliokuwa baruani aliyoiandika Chiku kwa Msiba anasema;
“Msiba ninakuaga, nakuachia msiba.” (ukurasa 47)

  

Ukweli kinzani katika sitaki iwe siri
Mukhtasari wa sitaki iwe siri
Sitaki Iwe Siri ni kazi ya fasihi ya watoto iliyoandikwa na Matundura mwaka wa 2008. Kazi hii imeangazia suala kuu kuhusu ugonjwa wa Ukimwi. Aidha, mwandishi ametumia wahusika mbalimbali ili kutoa maoni mbalimbali kuhusu ugonjwa huu katika jamii. Haya yamedhihirika kupitia kwa Mwalongo ambaye ni nyanya ya mhusika mkuu Musa. Mtoto wa Mwalongo (Yusuf) na mkewe Honorata walikufa kutokana na ugonjwa wa Ukimwi na kumwachia jukumu la ulezi wa wanawe watatu ambao ni Musa, Haki na Ukwa. Watoto hawa walipoendelea kukua, waliishi kumwuliza nyanya yao kilichosababisha kifo cha wazazi wao. Nyanya yao aliwaeleza kuwa ni ugonjwa ambao haukuwa na tiba. Watoto hawa walishangaa zaidi na kumwuliza nyanya yao kuhusu ugonjwa huo lakini nyanya yao alitaka iwe siri milele. Alijua kuwa katika jamii, wagonjwa wa Ukimwi waliepukwa kama wagonjwa wa ukoma na hivyo suala hili lilileta unyanyapaa katika jamii.
Hata hivyo, asubuhi moja ya siku ya Jumatatu, mwalimu mkuu, Bwana Said Selemani wa shule ya msingi ya Hekima alikuja na gazeti gwarideni na kuwatangazia wanafunzi kuwa kutakuwa na shindano la uandishi wa insha kuhusu ugonjwa wa Ukimwi na kuwa atakayeibuka mshindi atatuzwa na Wizara ya Afya ikishirikiana na Shirika la Afya siku ya kuathimisha siku ya Ukimwi ulimwenguni. Musa alifurahia sana baada ya kusikia tangazo hili na kwa ujasiri mwingi alitembea hadi ofisini kwa mwalimu mkuu na kumweleza kuwa angependa kushiriki katika shindano hilo. Mwalimu mkuu alifurahishwa na ujasiri wa Musa na kumwahidi kuwa angemsaidia kwa lolote atakalo. Anamtolea makala ya gazeti yenye tangazo hilo na kumtakia la heri katika uandishi wake. Jioni hiyo, Musa alienda katika maktaba ya shule na kumwomba mkutubi wa maktaba Bi. Maria amsaidie na makala yaliyoandikwa kuhusu Ukimwi. Bi. Maria alimweleza kuwa maktaba ya shule haina makala kuhusu Ukimwi na kumshauri Musa atembelee maktaba ya umma mjini huenda akafaidika huko. Musa alimshukuru Bi. Maria na kuondoka. Baadaye, alimweleza nyanya yake kuhusu nia yake ya kuandika insha na nyanya aliamua kumsaidia kadri awezavyo. Musa alianza utafiti wake hadi akaenda kumwona Dkt. Ataya katika hospitali ya wilaya ya Kericho. Dkt. Ataya alimsaidia Musa na kumpa majibu ya maswali kama vile namna ya kuambukizwa ugonjwa wa Ukimwi, jinsi ya kuueneza, njia za kuzuia na hata jinsi ya kutangamana na wagonjwa wa Ukimwi.
Hatimaye, Musa aliandika insha yenye mada Sitaki Iwe Siri na kumkabidhi Bi. Rosa Mistika ambaye alikuwa mwalimu wake wa Kiswahili aliyeikosoa. Baada ya kuikosoa, Musa aliituma kwa posta na kungojea matokeo. Musa alipata matokeo kuwa utungo wake ndio uliokuwa bora zaidi na alitunukiwa zawadi kemkem na pia aliiletea shule yake sifa tele. Hatimaye, siku ya kutuzwa kwa Musa, alipoombwa ahutubie umati, alimwalika nyanya yake Mwalongo pia ahutubu na Mwalongo alitoboa siri mbele ya umati kuwa ugonjwa ule wa Ukimwi ndio uliowaua wazazi wa Musa na ndugu zake miaka kumi iliyopita. Siri aliyoitaka nyanya Mwalongo iwe siri kwa muda huo wote inafichuka na kuwa si siri tena.

Ukweli kinzani katika sitaki iwe siri
Mbinu ya ukweli kinzani imetumika kama ifuatavyo katika kazi hii ili kufanikisha utunzi wa kazi inayojenga motifu ya siri;
Kwanza, Musa anapoamka asubuhi anafikiria namna mambo yangelikuwa iwapo wazazi wake wangelikuwa hai. Hata hivyo, fikra zile hazipeleki mbali kwa kuwa hata kilichowaua wazazi wake hakijui. Fikra zile zinamletea majuto kwa kuwa anaonelea kuwa wazazi wake wangekuwa hai angeweza kulala na kufurahia usingizi ila kwa sasa hawezi kwa sababu ana ndugu zake wadogo wanaomtegemea. Katika fikra zile, pana matumizi ya mbinu ya ukweli kinzani inayoendeleza motifu ya siri. Je, kwa nini Musa anatamani kulala na kufurahia usingizi ilhali yeye ni mwanafunzi anayefaa kuamka mapema ili aende shuleni? Ni nini kilichowaua wazazi wake na kumsababishia Musa majuto ya laiti angalikuwa na wazazi wake? Kwa nini mtoto mdogo ategemewe na wengine wadogo wake? Haya yote ni baadhi ya maswali ambayo yanaweza kumpitikia msomaji baada ya kusoma sehemu hii:
“Laiti wazazi wangu wangalikuwa hai, nami ningalipata fursa ya kulala na kufurahia usingizi jinsi wanavyofurahia watoto wengine wenye wazazi. Maskini siwezi kufanya hivyo kwa sababu wadogo zangu na nyanya yangu wananitegemea mimi.” (Ukurasa 1)
Aidha, nyanya yake Musa, Bi Mwalongo anajua kile kilichomuua mwanawe Yusufu na mkewe Honorata. Baada ya wajukuu wake kuondoka kwenda shuleni, anapatwa na fikra kuhusu kile kilichomuua mwanawe na mkasa mwanawe. Kwake, anataka sababu za kifo kile ziwe siri kwa wajukuu wake. Hata hivyo, wajukuu wale wanamsumbua kwa maswali kuhusu kifo cha wazazi wao kila wakati. Wanamwuliza;
“Kwa nini tunaishi na wewe? Wazazi wetu walikwenda wapi…Ni maradhi gani yaliyowaua wazazi wetu?” (Ukurasa 7)
Kwa hivyo, kwake Mwalongo, anataka chanzo cha kifo cha wanawe kiwe siri lakini wajukuu wake hawataki iwe siri. Haya ni kutokana na msimamo wa jamii kuhusu maradhi yaliyowaua wanawe yaliyochukuliwa kama laana kubwa kwa jamii.
Vilevile, nyanya ni kikale. Katika jamii nyingi za Kiafrika inajulikana kuwa nyanya ni wazee ambao hawana nguvu na hawawezi kujifanyia jambo lolote labda wafanyiwe na wanao. Haya ni kinyume na ilivyo kama mwandishi anavyomchora Bi. Mwalongo na namna anavyojifanyia kazi yake. Anasema;
“Nyanya Mwalongo alikuwa na umri wa miaka sitini hivi. Nywele zake kichwani zilikuwa zimebadilika na kuwa nyeupe kama theluji. Mwili wake ulikuwa umevamiwa na makunyanzi kwa sababu ya uzee. Mgongo wake ulikuwa umepinda kama uta na alilazimika kutembea kwa mkongojo. Nyanya Mwalongo alikuwa amekula chumvi nyingi.” (Ukurasa 7-8)
Taswira hii inaonyesha kuwa nyanya Mwalongo ni mwenye bidii licha ya umri wake na haya ni kinyume na matarajio katika jamii. Mwandishi anaeleza kuwa;
“Nyanya hatimaye aliondoka mahali pale alipokuwa amesimama kwa muda mrefu na kukumbuka maafa hayo yaliyomkumba miaka kumi iliyopita. Akaingia nyumbani akachukua jembe na kujikokota kwenda kondeni huku amelibeba jembe hilo begani. Licha ya umri wake mkubwa, nyanya Mwalongo alijikaza kwenda shambani kulima, la sivyo wajukuu wake wangekosa chakula. (Ukurasa 12-13)
Aidha, kadri wajukuu wake walivyoendelea kukua ndivyo aliendelea kutatizika roho. Hiki ni kinyume kwa sababu, katika jamii ya kawaida na uhalisia wa maisha, nyanya alifaa kufurahishwa na kukua kwa wajukuu wake kwa kuwa sasa wangeweza kujitegemea. Jambo linalomtatiza moyo ni kuhusu maradhi yaliyosababisha kifo cha wazazi wa wajukuu wake. Analo jibu la swali hili na anaulizwa na watu wanaofaa kujibiwa kwa kuwa wao pia waliathirika moja kwa moja lakini hataki kulijibu. Mwandishi anaeleza kuwa;
“Kutokana na misimamo hii, nyanya Mwalongo aliamua kuficha jibu la swali la wajukuu zake. ‘Nataka iwe siri, nyanya akaapa kuhifadhi moyoni mwake siri kuhusu aina ya maradhi yaliyowaua wazazi wa wajukuu zake.” (Ukurasa 12)
Ugonjwa ni kikale pia. Mtu anapogonjeka katika jamii anafaa kuchungwa vizuri na kutuzwa na kila mtu katika jamii. Aidha, anafaa ahurumiwe na asaidiwe kwa hali na mali. Hata hivyo, matarajio haya ni kinyume na inavyoonekana katika Sitaki Iwe Siri. Katika kazi hii mwandishi anachora unyanyapaa unaojitokeza katika jamii baada ya mtu kuugua ugonjwa wa ukimwi. Kupitia kwa maelezo ya nyanya, mwandishi anasema;
“Nyanya Mwalongo alipata taabu sana kulijibu swali hili. Ugumu wa kulijibu swali lenyewe ulitokana na msimamo wa jamii kuhusu maradhi yaliyowaua wazazi wa wajukuu zake. Maradhi yenyewe yalichukuliwa kuwa ni laana kubwa kwa jamii. Kila aliyeugua maradhi haya alianza kuepukwa kama mgonjwa wa ukoma. Akaogopwa jinsi yanavyoogopwa maiti. Akabaguliwa na jamii. Maradhi yenyewe yakachukuliwa kuwa ni muhuri wa mauti kwa kila aliyekumbwa na mkosi wa kuambukizwa.” (Ukurasa 11-12)
Haya pia yanajitokeza katika insha ya Sitaki iwe siri aliyoiandika Musa. Katika utungo huu, Musa anasema;
“Msichana huyu aliyeshangiliwa na kuonewa staha na kila mwanamume na hata wasichana wenzake kumwonea gere. Alianza ghafla kupungiwa mikono. Hakuna hata mtu mmoja aliyetaka kumsalimia kwa mkono kwa kuhofia kuambukizwa maradhi.” (Ukurasa 45)
Baada ya Musa kuamua kufanya utafiti juu ya ugonjwa wa Ukimwi ili aandike insha ambayo baadaye ilimletea ushindi, alimjulisha nyanya yake kuhusu mradi wa insha aliyokuwa anajiandaa kuiandika kisha akamwomba ruhusa ya kwenda katika Hospitali ya Wilaya ya Kericho ili aweze kuzungumza na daktari ambaye angeweza kumpa habari kuhusu Ukimwi. Nyanya anapoyasikia haya anashangaa badala ya kuufurahia ujasiri wa mjukuu wake. Aliwaza;
“Siri ambayo nimekuwa nikiiweka jinsi kaburi linavyohifadhi siri hatimaye itajulikana.” (Ukurasa 27)
Anapoendelea na utafiti kuhusu suala la Ukimwi, Musa anagundua kuwa kuna ukinzani wa mwonoulimwengu kuhusu suala la Ukimwi na jinsi hali halisi ilivyo. Wakati ulimwengu unapochukulia wagonjwa wa Ukimwi kuwa kama wagonjwa wa ukoma wanaopaswa kuepukwa, waliolaaniwa na waliotiwa muhuri wa mauti, hali halisi kupitia kwa daktari inadhihirisha kinyume cha haya. Musa anapomwuliza daktari kuhusu chanzo cha ugonjwa wa Ukimwi, namna ya kujikinga na jinsi ya kutangamana na wagonjwa wa Ukimwi, Dkt. Ataya anamweleza kuwa;
“UKIMWI SI UCHAWI… kuna njia nyingi kupitia kwazo mtu anaweza kuambukizwa Ukimwi… kufanya mapenzi kabla ya ndoa na bila kinga… kwenda hospitalini na kudungwa sindano ambayo imetumiwa kumdunga mtu mwingine ambaye ameambukizwa virusi vinavyosababisha Ukimwi… na hata vifaa vyote vyenye makali kama vile visu na nyembe ambazo zinatumiwa kutahirisha…kutiwa damu yenye virusi hivyo… Mtoto baada ya kuzaliwa kunyonya maziwa ya mama yake…” (Ukurasa 37-41)
Kuhusu tiba ya ugonjwa wa Ukiwmi Dkt. Ataya alisema;                                                 
“Hadi sasa hakuna tiba yoyote kwa maradhi ya Ukimwi, ingawa kuna dawa ambazo wagonjwa wanaougua Ukimwi hutumia ili kupunguza athari za ugonjwa huo. Isitoshe, lishe bora pia huwafaa wagonjwa wa Ukimwi.” (Ukurasa 42)
Mwishowe, daktari aliwatahadharisha kuwa kuna matapeli wanaowahadaa watu kwamba wana uwezo wa kutibu ugonjwa huo lakini hakukuwa na ushahidi wowote unaoweza kutegemewa kwamba waganga hao wana uwezo wa kuyatibu maradhi hayo. Alieleza kuwa waganga hao hutumia fursa hiyo kujipatia pesa kwa kuwa ni matapeli. Maelezo haya ni kinzani na anavyoeleza mwandishi kuwa;
“Nyanya alitumia raslimali nyingi kugharamia matibabu yao, lakini ndwele hiyo haikusikia dawa… hatimaye nyanya alienda kwa waganga wa mitishamba, tunguri na hirizi. Waganga hao wakajitahidi kadri ya uwezo wao hadi wakainua mikono.” (Ukurasa 9)
Katika insha aliyoiandika Musa kuna ukinzani wa namna Yuri alivyoanza kujipa raha na namna alivyomalizwa na ugonjwa wa Ukimwi. Musa anaeleza kuwa;
“Ajidhaniye kasimama, aangalie asianguke… Walijua bayana kuwa Yuri alikuwa ameanza kuanguka- tena kwa kishindo kikubwa… zimwi likujualo halikuli ukakwisha, hili lililompata Yuri wakati wa pitapita zake kwenye majumba ya starehe liliapa kumumaliza mara moja. Lilihakikisha kuwa Yuri alipitisha siku zake katika sayari hii iitwayo dunia kwa kasi ambayo hakuitarajia.” (Ukurasa 45)
Kwa hivyo, inaonekana kuwa matarajio ya Yuri yalikwenda kinyume kabisa. Hakutarajia kuepukwa na marafiki wala kudhoofika kiafya. Alifikiria kuwa marafiki wake wangesimama naye kwa dhiki na faraja lakini kinyume chake wanamwepuka.
“Dhihaka za watu hasa marafiki zake kuwa Yuri alikuwa amekwisha kazi na hata kutemewa mate zilimtesa sana.” (Ukurasa 48)
Kutokana na kero ya moyoni aliyopata Yuri kutoka kwa marafiki zake, badala ya kuanza kutumia dawa za kupunguza athari za ugonjwa wa Ukimwi mwilini mwake, Yuri anaamua kujiua. Anapojiua, anaacha kijikaratasi chenye maandishi yafuatayo;
“Sitaki iwe siri. Nimejiua kwa sababu ya Ukosefu wa Kinga Mwilini. Maisha yangu ingawa nimeyakatiza na
                                                                   yawe funzo kwa wengine.”
                                                                            (Ukurasa 48)                                         
Mwisho, kwenye mkutano wa kumtunza Musa kwa sababu ya ushindi wake, mambo yanakwenda kinyume na yanavyotarajiwa. Kwanza, Musa anaenda kinyume na matarajio ya umati kwa kusema kuwa ushindi sio wake pekee bali ni wa kila mtu. Haya yanadhihirisha kuwa Musa ni shujaa na hajipendi. Anatambua mchango wa wengine waliochangia kuleta ufanisi wa kazi yake. Aidha, siri aliyokuwa ameamua kuificha Bi. Mwalongo milele inafichuka. Licha yake kuapa kuwa anataka siri ya ugonjwa uliowaua wazazi wa wajukuu wake ibaki kuwa siri hadi kaburini, anafichua siri hiyo hadharanikwa kusema;
“Ni sadfa kwamba siri niliyoighubika kwa miaka mingi ili wajukuu zangu wasiijue imefichuliwa. Wajukuu wangu hawa ni mayatima. Wazazi wao walifariki kutokana na maradhi ya Ukimwi, nao wakabaki mikononi mwangu. Waliponiuliza kilichowaua wazazi wao, niliwajibu kuwa ni maradhi. Walipotaka kujua ni maradhi yepi, nilidinda kuwaambia. Nilitaka iwe siri. Lakini sasa Musa huyu ameandika insha ya ushindi Sitaki iwe siri.” (Ukurasa 65)


5. Hitimisho na mapendekezo
Hitimisho
Kutoakana na uchanganuzi huu ni dhahiri kuwa mbinu ya ukweli kinzani imetumika pakubwa katika ujenzi wa motifu ya siri katika kazi teule. Licha ya kazi hizi kukinzana katika uteuzi wa mada ambazo ni Nataka Iwe Siri na Sitaki Iwe Siri, kazi hizi zimezidi kuendeleza mbinu hii katika ujenzi wa wahusika wanaoendeleza mawazo makuu ya waandishi hawa kuhusu siri. Huku baadhi ya wahusika wakitaka iwe siri, wengine hawataki iwe siri na wanaifichua hadharani. Aidha, baadhi ya wahusika wanaotaka iwe siri wanaifichua siri hiyo. Wanaotaka iwe siri na hatimaye kuifichua wanatenda kinyume na matarajio kwa sababu, iwapo mtu binafsi anataka iwe siri anafaa kuiweka milele hadi afe, yaani iwe siri sirini. Aidha, uchanganuzi wa data umeonyesha kuwa siri huwa siri kwa mtu binafsi. Hakuna siri ya watu wawili. Ikiwa mtu wa kwanza ataamua kumfichulia siri mtu wa pili siri yake, afahamu kuwa hiyo haitakuwa siri tena kwa sababu mtu wa pili anaweza kumtobolea mtu wa tatu siri ya mtu wa kwanza na msururu ukaendelea vivyo hivyo hadi siri ile ikajilikana na watu wengi zaidi ya alivyotarajia mwenye siri. Kwa hivyo, Nataka Iwe Siri na Sitaki Iwe Siri ni kazi ambazo zimeonyesha matumizi ya mbinu ya ukweli kinzani katika ujenzi wa wahusika wanaoiendeleza motifu ya siri.


Mapendekezo
Makala haya yameangazia matumizi ya mbinu ya ukweli kinzani inayotumiwa na wahusika tofauti ili kuendeleza motifu ya siri. Hii ni mbinu moja tu kati ya mbinu zingine nyingi za uandishi. Kwa hivyo, wahakiki wa baadaye wanaweza kuangazia namna ambavyo mbinu zingine za uandishi kama vile kisengere mbele, kisengere nyuma, taswira na taharuki zimetumiwa na waandishi hawa ili kuendeleza motifu ya siri.
Vilevile, kazi hii imeangazia kazi teule za Nataka Iwe Siri na Sitaki Iwe Siri. Wahakiki wa baadaye wanaweza kuangazia namna ambavyo mbinu hii ya ukweli kinzani imetumika kuendeleza motifu ya siri katika kazi zingine zilizoandikwa kwa kuzingatia motifu hii. Kazi hizi ni kama vile Siri Sirini, Siri Ya Baba Yangu, Siri na Siri ya Ging’ing’i.


Marejeleo
Abrams, M. H. A. (1981). Glossary of Literary Terms. New York: Holt, Rinehart and Winston.
Coyle, M. na Wengine. (1990). Encyclopedia of Literature and Criticism. London: Macmillan.
Cuddon, J. A. (2013). A Dictionary of Literary Terms and Literary Theory. Wiley: Blackwel.
Eagleton, T. (1983). Literary Theory: An Introduction. Oxford: Basil Blackwell.
Frazer, G. J. (1959). The New Golden Bough. New York: Criterion Books.
Fyre, N. (1957). Anatomy of Criticism. Princeton University Press.
Gathara, F. K. (2015). Taswira ya Jagina Katika Tendi: Ulinganishi wa Fumo Liyongo na Nabii Isa. Tasnifu ya         Uzamili                Katika Chuo Kikuu cha Nairobi (Haijachapishwa).
Jung, C. G. (1957). The Archetypes and The Collective Unconsious. London: Routledge and Kegan Paul Ltd.
Jung, C. G. (1972). Four Archetypes: Mother, Rebirth, Spirit, Trickster. London: Routledge & Kegan Paul Ltd.
Karama, M., Mutiso, K. na Chimerah, R. (2018). Ushairi wa Kisufi Katika Tendi za Kale za Kiswahili: Mfano Wa     Utendi wa Siri La Asrari. Katika Mara Research Journal of Kiswahili Vol. 3, No. 1.The African Premier  Research Publishing Hub.
Kilonzo, J. na Masaku, M. (2017). Mwongozo wa Tumbo Lisiloshiba na Hadithi Nyingine. Globalink Publishers.       Nairobi: Kenya.
Kirumbi, P. (1971). Nataka Iwe Siri. Tanzania: Printpak Publishers.
Matundura, B. (2008). Sitaki Iwe Siri. Nairobi: Longhorn Publishers
Matundura, B. (2018). Motifu ya ‘Siri’ Katika Fasihi ya Kiswahili na Jinsi Inavyoendeleza Dhamira ya       Mwandishi. Taifa Leo. Novemba 21.
Mulokozi, M. M. (1996). Utangulizi wa Fasihi ya Kiswahili. Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili: Dar es Salaam.
Mutiso, K. (1999). Sira ya Majagina Buddha na Muhammed. Swahili Kolloquim Universitat. Bayreuth. Mei 14-15,               1999.
Njogu, K. na Wafula, R. (2007). Nadharia za Uhakiki wa Fasihi. Nairobi: JKF.
Wamitila, K. W. (2002). Uhakiki wa Fasihi. Nairobi: Phoenix Publishers.
Werner, A. (1968). Myths and Legends of the Bantu. London: Frank Cass & Company Limited.
Yenjela, W. (2015). Pathways to African Feminism and Development; Invoking Memories of Legendary African      Women’s Studies Centre. Vol.1. (3). University of Nairobi.









No comments:

Post a Comment